1 Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno,

2 kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu.

3 Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi.

4 Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu.

5 Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao.

6 Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Ninyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote.