1 Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi.

2 Tangu sasa, basi, maisha yaliowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, si na tamaa za kibinadamu.

3 Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu.

4 Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni.

5 Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu wazima na wafu!