1 Ndugu, ninyi wenyewe mnafahamu kwamba ziara yetu kwenu haikuwa bure.

2 Mnajua jinsi tulivyodhulumiwa na kutukanwa kule Filipi kabla ya kufika kwenu Thesalonike. Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema yake.

3 Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote.

4 Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani.

5 Ninyi mnajua kwamba sisi hatukuja kwenu na maneno matamu ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi!

6 Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote,

7 ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa Wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake.

8 Tuliwapenda ninyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu!

9 Ndugu, mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika. Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu.

10 Ninyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, jinsi mwenendo wetu kati yenu ninyi mnaoamini ulivyokuwa mzuri, mwadilifu na usio na lawama.

11 Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe.

12 Tuliwapeni moyo, tuliwafarijini na kuwahimiza ili mpate kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye aliwaiteni mshiriki Utawala na utukufu wake.

13 Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, ninyi mliusikia mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.

14 Ndugu, ninyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Ninyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi,

15 ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni adui za kila mtu!

16 Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia.

17 Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye, tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena!

18 Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo, nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia.

19 Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni ninyi wenyewe; ninyi ndio tumaini letu na furaha yetu.

20 Naam, ninyi ni utukufu wetu na furaha yetu!