11 Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga.
12 Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa ninyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni.
13 Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu.
14 Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake.
15 Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao.
16 Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena.
17 Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.
18 Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, akatupa nasi jukumu la kuwapatanisha watu naye.
19 Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye.
20 Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.
21 Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.