1 Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana

2 msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba Siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu.

3 Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana Siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule Uasi Mkuu utokee na yule Mwovu aonekane ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa.

4 Yeye atapinga kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu. Naam, hata ataingia na kuketi ndani ya Hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu.