1 Kisha nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
2 Akalikamata lile joka--nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani--akalifunga kwa muda wa miaka elfu moja.
3 Malaika akalitupa Kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka elfu moja itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu.
4 Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumtangaza Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa muda wa miaka elfu moja.
5 (Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka elfu moja itimie.) Huu ndio ufufuo wa kwanza.
6 Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.
7 Wakati miaka elfu mia moja itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake.
8 Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani.
9 Walitawanyika katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watu wa Mungu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza.
10 Ibilisi, aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele.
11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena.
12 Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uzima, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo.
13 Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; kifo na kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake.
14 Kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili.
15 Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto.