1 Ninyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu.

2 Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu.

3 Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu.

4 Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika,

5 hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa.

6 Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni.

7 Ndivyo alivyopenda kuonyesha kwa watu wa nyakati za baadaye, ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu.

8 Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu.

9 Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.

10 Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.

11 Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine--mnaoitwa, "wasiotahiriwa" na Wayahudi ambao hujiita, "Waliotahiriwa," (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao)--kumbukeni mlivyokuwa zamani.

12 Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini Mungu hapa duniani.

13 Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo.

14 Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui.

15 Aliiondoa ile Sheria ya Wayahudi pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani.

16 Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu.

17 Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu.

18 Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba katika Roho mmoja.

19 Basi, ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu.

20 Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi.

21 Yeye ndiye mwenye kulitengeneza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya B wana.

22 Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.