10 Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.

11 Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi.

12 Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza.

13 Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti.

14 Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani,

15 na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu.

16 Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.

17 Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu.