1 "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.

2 Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi.

3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni.

4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. ic

5 "Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.

6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue.

7 Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa.

8 Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.