46 Naye Maria akasema,

47 "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

48 Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

49 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.

50 Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.

51 Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

52 amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.

53 Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

54 Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.

55 Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."