7 Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa.
8 Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, "Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka."
9 Nao wakamwuliza, "Unataka tuiandae wapi?"
10 Akawaambia, "Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia.
11 Mwambieni mwenye nyumba: Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?
12 Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo."
13 Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.
14 Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake.