18 Mara watu wakaja wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani wamweke mbele ya Yesu.
19 Lakini kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya dari, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu.
20 Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, "Rafiki, umesamehewa dhambi zako."
21 Walimu wa Sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: "Nani huyu anayemkufuru Mungu kwa maneno yake? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!"
22 Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, "Mnawaza nini mioyoni mwenu?
23 Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, Umesamehewa dhambi, au kusema, Simama utembee?
24 Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kusamehe dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Simama, chukua kitanda chako uende zako nyumbani."
25 Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda zake nyumbani huku akimtukuza Mungu.