1 Baada ya kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu.

2 Huko kulikuwa na jemadari mmoja Mroma ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu kufa.

3 Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje amponye mtumishi wake.

4 Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: "Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo,

5 maana analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi."

6 Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu kufika nyumbani kwa yule jemadari Mroma, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: "Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu.

7 Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako; amuru tu, na mtumishi wangu atapona.

8 Mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, Nenda!, naye huenda; namwambia mwingine, Njoo! naye huja; na nikimwambia mtumishi wangu, Fanya hiki!, hufanya."

9 Yesu aliposikia hayo, alishangaa; halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, "Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli."

10 Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa.