24 Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: "Mlikwenda kule jangwani, hivi mlitaka kuona kitu gani? Mlitaka kuona unyasi unaotikiswa na upepo?
25 Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevalia mavazi maridadi? La hasha! Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme!
26 Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
27 Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: Hapa ni mtumishi wangu, asema Bwana; ninamtuma akutangulie, akutayarishie njia."
28 Yesu akamalizia kwa kusema, "Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko yeye."
29 Waliposikia hayo watu wote na watoza ushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane.
30 Lakini Mafarisayo na walimu wa Sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu wakakataa kubatizwa na Yohane.