31 Yesu akaendelea kusema, "Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani?

32 Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine: Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza! Tumeomboleza, lakini hamkulia!

33 Kwa maana Yohane alikuja, yeye alifunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: Amepagawa na pepo!

34 Akaja Mwana wa Mtu; anakula na kunywa, mkasema: Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi!

35 Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali."

36 Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani mwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula.

37 Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa anaishi maisha mabaya. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.