1 Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza.
2 Humo baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya sabato ili wapate kumshtaki.
3 Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, "Njoo hapa katikati."
4 Kisha, akawauliza, "Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?" Lakini wao hawakusema neno.
5 Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, "Nyosha mkono wako!" Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena.