24 Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

25 Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake.

26 Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.

27 Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, Mheshimiwa, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?

28 Yeye akawajibu, Adui ndiye aliyefanya hivyo. Basi, watumishi wake wakamwuliza, Je, unataka twende tukayangoe

29 Naye akawajibu, La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia.

30 Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu."